Viongozi kutoka mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani G20 wanaendelea kuwasili katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia leo kwa mkutano wa baada ya janga la UVIKO-19 uliotawaliwa na msuguano kati ya Marekani na China.
Mkutano huo wa G20 unatokea katika wakati ambapo watu kutoka kila pembe ya dunia wanakabiliwa na gharama kubwa ya maisha ikiwemo kupanda kwa bei za vyakula na mafuta, mzozo wa vita nchini Ukraine na tishio la matumizi ya silaha za nyuklia.
Ni mkutano mkubwa zaidi wa viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda tangu kuanza kwa janga la ugonjwa wa UVIKO-19, hata hivyo sio mkutano wenye kupendeza.
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, ambaye anahudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani, ametoa wito kwa mataifa yenye nguvu duniani kuungana dhidi ya unyonyaji wa uchumi wa dunia unaofanywa na wale aliowaita “watendaji wabaya.”
Baada ya kuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Uingereza ndani ya mwaka mmoja, Sunak anatarajiwa kuwa na mkutano wake wa kwanza na Rais wa Marekani Joe Biden pamoja na viongozi wengine wa dunia katika mkutano wa kilele kisiwa cha Bali, Indonesia.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ushindani kati ya China na Marekani umeongezeka kwa kasi. Beijing inaonekana kuwa na nguvu na yenye ushawishi na inapambana kwa udi na uvumbi kuwa taifa lenye nguvu kubwa duniani na kuchukua nafasi ya Marekani.
Rais Biden na Xi wanatarajiwa kuwa na mazungumzo pembezoni mwa mkutano huo ambapo Biden amegusia kuhusu mkutano huo na Xi, na kutahadharisha juu ya kuvuka mstari mwekundu wa kila nchi kwa matumaini kwamba, ushindani kati yao hautakuwa chanzo cha nchi hizo mbili kuingia kwenye makabiliano na migogoro.
Xi, anatajwa kuwa huenda asiwe msaada mkubwa kwa Marekani. Anaingia kwenye mkutano huo na Biden baada ya kuchaguliwa kwa muhula wa tatu wa kihistoria hivi karibuni na kumfanya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi wa China.
Katika meza ya mazungumzo huko Bali nchini Indonesia, hatokuwepo Rais wa Urusi Vladimir Putin, kutokana na Uvamizi wake wa kijeshi nchini Ukraine kumeifanya safari ya Bali kuingia doa, Badala yake Rais huyo amemtuma waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov kumwakilisha.