Sudan huenda ikaishiwa dawa, mafuta na ngano baada ya maandamano ya kisiasa kulazimisha kufungwa kwa bandari kuu iliyopo mashariki mwa nchi,
Taarifa hiyo imethibitishwa na baraza la Mawaziri nchini humo.
Watu wa kabila la Beja ambao wanaishi mashariki mwa Sudan, walifunga barabara na kusababisha bandari za bahari ya Sham kufungwa katika wiki za karibuni, yakiwa maandamano dhidi ya kile wanachosema ni ukosefu wa nia ya kisiasa ya utawala na hali mbaya ya kichumi katika eneo lao.
Baraza la mawaziri limesema linatambua madai ya watu wa mashariki mwa Sudan na kusisitiza haki ya kufanya maandamano ya amani, lakini limeonya kwamba kufungwa kwa bandari ya Sudan na barabara kuu zinazounganisha mashariki na nchi nzima kunahujumu maslahi ya watu wa Sudan.
Aidha baraza hilo limeahidi kutafuta suluhu ya kisiasa kwa matatizo ya watu wa mashariki mwa Sudan na limewataka waandamanaji kuanza majadiliano na serikali.
Waandamanaji waliahidi mwezi uliopita kuruhusu tena usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Sudan kusini kupitia kituo cha kwenye bahari ya Sham.Walilazimisha pia kufungwa kwa bomba la mafuta ambalo linapeleka mafuta ghafi kwenda mji mkuu Khartoum.