Mshambuliaji kutoka nchini Burundi na klabu ya Namungo FC Bigirimana Blaise, atakosa michezo miwili ya nyumbani na ugenini ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Clube Desportivo 1º de Agosto ya Angola, utakayochezwa mwezi ujao.
Daktari wa timu ya Namungo FC, Gabriel Kasonde amesema Blaise atakosa michezo hiyo ya kimataifa, kufuatia majeraha ya mguu yanayomsumbua kwa sasa.
Blaise alipata majeraha hayo kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba SC, uliochezwa Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja – Zanzibar , huku Namungo FC ikikubali kichapo cha mabao mawili kwa moja.
Kasonde amesema mbali na kukosa michezo hiyo ya kimataifa, mshambuliaji huyo anatarajia kukaa nje ya uwanja wa kipindi kisichopungua miezi mitatu.
“Atakaa nje ya uwanja wiki tatu kisha anaweza kukaa nje ya uwanja miezi mitatu wakati akirejea kwenye ubora wake taratibu na itategemea na namna hali yake itakavyokuwa.” Amesema Kasonde.
Namungo FC itaanzia ugenini nchini Angola Februari 14 dhidi ya Clube Desportivo 1º de Agosto, kabla ya kumalizia mchezo wa mkondo wa pili hapa nyumbani Tanzania Febriari 21.
Mshindi wa jumla ya michezo hiyo miwiwli atatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.