Joaquín Guzmán, maarufu kama El Chapo ambaye anafahamika kama bilionea wa biashara za dawa za kulevya na silaha, amekutwa na hatia katika mashtaka yote kumi yaliyokuwa yanamkabili mbele ya Mahakama ya New York nchini Marekani.
El Chapo mwenye umri wa miaka 61, alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya kumiliki mtandao mkubwa wa biashara ya dawa za kulevya, kufanya biashara haramu ya silaha pamoja na utakatishaji fedha.
Ingawa bado hajahukumiwa adhabu kutokana na makosa hayo, lakini kutokana na sheria za Marekani, anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Bilionea huyo alikamatwa Januari 2016 baada ya kutoroka katika jela yenye ulinzi mkali nchini Mexico miezi mitano kabla. Alisafirishwa kwenda nchini Marekani ambapo aliwekwa rumande kwenye jela yenye ulinzi zaidi na kufikishwa mahakamani.
Mwendesha Mashtaka aliiambia Mahakama kuwa Guzman alikuwa anamiliki mtandao mkubwa zaidi duniani uliokuwa unaingiza kiasi kikubwa zaidi cha dawa za kulevya nchini Marekani.
-
Ughaibuni: Mtanzania akamatwa na dawa za kulevya tumboni
-
Solskjaer afunguka baada ya kupigwa na PSG nyumbani
Hata hivyo, Guzman hakuonesha ishara yoyote ya kushtushwa na hukumu hiyo ya Mahakama iliyosomwa na Jaji Judge Brian Cogan. Mwanasheria wake alieleza kuwa wanapanda kukata rufaa.
Chanzo: Aljazeera