Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema katika Bajeti Kuu ya Serikali takriban Shilingi Bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa.
Bashungwa amesema hayo Juni 14, 2021 Jijini Mwanza katika ziara ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo ameeleza kuwa Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango zinaendelea na utaratibu wa kurudisha bahati nasibu ya Taifa ili mapato yaende kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo.
“Mhe. Rais, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi ya kusalimia, na naomba nianze na habari njema kwamba jana timu yetu ya Taifa iliicharaza timu ya Malawi mabao mawili kwa sifuri” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameongeza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu zimeanza kusimamia kwa pamoja michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA inayofanyika kitaifa mkoani Mtwara ili kupata wanamichezo wenye vipaji mbalimbali ambao watasaidia Taifa kuwa na timu zenye ushindani na ufanisi mzuri kitaifa na kimataifa.
Ametumia nafasi hiyo pia kumshukuru Rais Samia kwa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye nyasi bandia nchini ili miundombinu ya michezo iweze kupendeza na kuwa katika hali nzuri ambapo kwa kuanza italenga viwanja vya majiji na kadiri fedha itakavyopatikana viwanja vya kwenye Manispaa na Halmashauri vitafikiwa.
Aidha, Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Wasanii nchini pamoja na Wanahabari kwa kazi nzuri wanazofanya kwa maslahi ya Taifa ambapo amewataka kuendelea kumuunga mkono Rais katika kuleta maendelo endelevu nchini.