Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa bandari ya uvuvi wilayani Kilwa, Lindi ambao utasaidia kuongeza kasi ya uvuvi wa kisasa na biashara ya samaki ili kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo. 

Ameyasema hayo leo Oktoba 6, 2021 wakati akizungumza na watumishi, madiwani na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika mkoa wa Lindi.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amesema mradi huo unatarajia kuchangia ukuaji wa maendeleo kwa wananchi wa wilaya ya Kilwa na Watanzania kwa ujumla, hivyo amewataka wananchi wachangamkie fursa hiyo kwa kujenga nyumba za kulala wageni, migahawa kwani baada ya kukamilika watu wengi watahitaji makazi.

Wataalamu walishapita katika maeneo yote ya pwani kuanzia pwani ya kutokea Tanga hadi Mtwara na kuridhia kwamba Kilwa ni mahali sahihi kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo kwani eneo la uwanda wake ni zuri na lina kina kirefu ambacho hakihitaji kuongezwa na Mheshimiwa Rais ameridhia ijengwe,” Amesema Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa.

Baada ya Waziri Mkuu kutoa agizo hilo wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa waliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia kwa kuamua kujenga bandari hiyo katika wilaya yao kwa sababu mradi huo unakwenda kuimarisha biashara ya samaki pamoja na kuongeza ajira.

Mariam Yusufu ambaye ni miongoni mwa wakazi hao amesema amefurahishwa na uamuzi wa Rais Samia wa kutengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa bandari ya uvuvi wilayani Kilwa kwa kuwa mradi huo unakwenda kuboresha maendeleo yao pamoja na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana.

Taifa Stars yakamilisha maandalizi, kuivaa Benin
Mirabaha kuwanufaisha wasanii nchini