Bingwa wa mikanda ya dunia ya WBC, WBO, IBF Mwingereza Natasha Jonas amewafunda mabondia nchini namna alivyofanikiwa kufikia lengo lake la kucheza michuano ya Olimpiki, lengo likiwa kuwahamasisha wajitahidi kutimiza malengo yao.
Bondia huyo ameletwa nchini na Baraza la Michezo la Taifa (BM) chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambapo amekutana na mabondia wa ridhaa na wa kulipwa na kuzungumza nao.
Amesema katika Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1988 akiwa na umri wa miaka minne alifuatilia michezo ya ngumi akatamani na yeye siku moja kufika huko na ndoto yake ilitimia mwaka 2012 baada ya kushiriki na kufanya vizuri.
Baadhi ya mabondia wa Tanzania walimuuliza iwapo kama serikali ya Uingereza inawasapoti mabondia wa huko na yeye alisema kwa wale waliofikia hatua ya kuwakilisha taifa wamekuwa wakipewa sapoti kubwa hasa fedha za kufanya mambo yao.
Miongoni mwa mabondia waliokuwepo ni Ibrahim Class aliyesema anashukuru kwa kupata ufafanuzi mzuri kwani ameelewa kumbe mabondia wa ngumi za kulipwa hata Uingereza hawasapotiwi bali wanaotazamwa ni wale wa ridhaa.
Kwa upande wake, Abdallah Pazi Dula Mbabe amewashukuru BMT na Wizara ya Michezo kwa kuwaletea bondia huyo akisema wamejifunza kutoka kwake na kuwahimiza waendelee kuwaleta wengine pia katika mapambano makubwa wapambane nao.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Makore Mashaga amesema ushauri alioutoa Natasha unaonesha nchini kwao kuna misingi mizuri ya ngumi nddo maana wanafanikiwa.