Eve Godwin – Dodoma.
Hospitali ya Benjamin Mkapa – BMH, ya Jijini Dodoma inajipanga kupokea Mashine nyingine mpya ya kisasa itakayoimarisha utoaji wa huduma za Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tokushukai Medical Corporation, Dkt. Higashiue Shinichi.
Hayo yamebainishwa na Bingwa wa Upasuajia wa Mifumo ya Fahamu ya Uti wa Mgongo na Ubongo wa BMH, Dkt. Henry Humba ambaye amesema mbinu hiyo itapunguza gharama za matibabu, muda wa kuuguza jeraha na muda wa Daktari kufanya upasuaji na Madaktari Bingwa hao watapewa mafunzo ya Upasuaji huo kuanzia Oktoba 1-6, 2023 Hospitalini hapo.
“Tunatarajia kuwa na madaktari kutoka Hospitali za Benjamin Mkapa, Mnazi Mmoja NED Surgical Institute ya Zanzibar, Hospitali ya Mifupa (MOI), Mloganzila, Bugando, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Agha Khan. Tutaanza kwa mjadala wa kitaaluma utakaolenga kutathimini hali halisi ya utoaji wa huduma za Upasuji wa Mifumo ya Fahamu, Uti wa Mgongo na Ubongo.” alisema Humba.
Hata hivyo, amesema Mafunzo hayo yatadumu kwa siku tano na yataongozwa na madaktari bingwa wabobezi wa Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu kutoka nchini Japan ambao pia watashiriki kufanya Upasuaji na madaktari wazawa, ikiwa ni hatua za awali kuwezesha huduma hizo nchini.