Baraza la Michezo Tanzania (BMT), limebariki Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likisema: “Tunaitakia TFF uchaguzi mwema wenye amani, upendo na utulivu.”
Pamoja na baraka hizo, Baraza limeiagiza TFF kuwaelekeza wagombea wote kuzipitia sheria za Baraza la Michezo, Kanuni za Baraza na kanuni za Usajili, hususani kanuni ya 8 (1) na (2).
Kanuni hiyo ya 8 (1) na (2), inaagiza kuwa endapo wagombea wote watakaoshinda nafasi wanazowania kwa sasa ndani ya TFF, hawana budi kuachia nafasi mojawapo katika uongozi wa mpira kwa miguu katika ngazi ya wilaya au mkoa aliyoshinda awali.
BMT imetoa agizo hilo ikiwa ni kukumbushana juu ya utii wa sheria na kuepuka kushika nyadhifa mbili kwa wakati mmoja.
Katika barua yake iliyoandikwa Juni 19, mwaka huu na kusainiwa na Katibu Mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja, Baraza hilo limesema: “Uchaguzi huu usivuruge amani iliyopo nchini. Wagombea wakumbuke kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.”
Baraza limesisitiza kuwepo na haki katika mchakato mzima kuelekea kwenye uchaguzi. Uchaguzi na mchakato wake uwe huru na amani na usiwe ni kichocheo cha uvunjifu wa amani.
Baada ya viongozi kupatikana, watakula kiapo cha utii, na kujaza fomu Namba 5 ya BMT ya utekelezaji majukumu yao kama Kanuni ya 8 (4) inavyoeleza.
Kadhalika, mara baada ya uchaguzi, Baraza limeagiza kuhusisha baadhi ya vifungu vya sheria ya Baraza ili viendane na katiba za TFF na wadau pamoja na kanuni zao.