Nahodha na Mshambuliaji wa Simba SC John Bocco amesema pamoja na kutolewa katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Robo Fainali, hawana budi kujivunia kwa ubora wa kikosi chao.
Kikosi cha Simba SC kilirejea Dar es salaam jana Jumapili (Aprili 30) kikitokea Casablanca-Morocco ambako kilicheza dhidi ya Wydad AC ambayo imesonga mbele kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati 4-3, baada ya timu hizo kupata matokeo ya jumla ya 1-1.
Bocco amesema kikosi cha Simba SC kilionesha kuwa bora wakati wote kwa kutoa ushindani kwa timu zote walizokutana nazo msimu huu kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ambazo zilikuwa zikitajwa kuwa vigogo wa soka Barani humo.
“Hatukutarajia kupata matokeo haya lakini hata wapinzani wetu hasa katika mchezo wa marudiano na Wydad AC, hawakutarajia kama wanaweza kupata ushindi mwembamba kisha kufikia hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti,” amesema Bocco.
Bocco amesema baada ya kumaliza safari ya michezo ya Kimataifa, kikosi chao kinaelekeza nguvu katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kuivaa Azam FC.
Ameongeza kuwa anaamini Simba SC itafanya vizuri dhidi ya Azam FC na kufuzu Fainali ya ASFC ambayo mwaka huu itapigwa katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Simba SC ilifuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Msimamo wa Kundi C ikiwa na alama tisa, ikitanguliwa na Raja Casablanca iliyomaliza kwa kuwa na alama 13.
Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajiwa kushuka dimbani Mei 3, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC, utakaochezwa Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi kabla ya Mei 6, mwaka huu kukipiga na Azam FC mkoani Mtwara katika mchezo wa Nusu Fainali ASFC utakaochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona.