Nahodha na mshambuliaji wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC John Raphael Bocco, amekanusha taarifa za kuwa na tofauti na mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere.
Tofauti baina ya wawili hao zimeripotiwa kwenye mitandao ya kijamii kufuatia kitendo kilichoonekana jana wakati wakishangili bao la kwanza dhidi ya Polisi Tanzania, lililofungwa na kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama dakika ya 63.
Picha za Televisheni zilimuonyesha Bocco akimkwepa Kagere alipotaka kumkumbatia sanjari na mfungaji wa bao hilo, ambalo liliibua hamasa kubwa kwa wachezaji wa Simba SC, na baadae kupata bao la pili dakika ya 90.
Bocco ameandika kwenye ukurasa wake wa Istagram: “@mediekagere_officialaccount Hatuna tofauti yoyote na medi tupo sawa… walicho kitafsiri watu ni mihemko yao ya kilasiku yakukosa habari na kutaka kutengeneza story zisizo na kichwa wala miguu. Sina shida na medi na wala medi hana shida na mimi pia @mediekagere_officialaccount timu yetu hatuna tatizo lolote niamani na upendo hizo zilikua fikwa na hisia za watu kutafsiri na kuhisi vitu visivo kuwa na uhalisia na uwakika.”
Kabla ya ujumbe huo, Bocco aliandika ujumbe wenye maneno makali kupitia ukurasa wa Instagarm, na baadae aliufuta kwa kuhisi usingepokelea vizuri na jamii ya mashabiki wake wanaomfuata kwenye ukurasa huo.