Mkaguzi msaidizi wa Polisi, Magreth Kitundu, amewataka waendesha pikipiki za abiria maarufu kama Bodaboda kuacha kukimbiza vyombo vyao kwa mwendo kasi, ili kupunguza ajali za barabarani wanazo zisababishwa.
Kitundu alitoa wito huo wakati akitoa elimu ya usalama barabarani kwa bodaboda wa kijiwe cha njia panda ya Mafisa kwa Dala, kilichopo kata ya Tungi Wilaya na Mkoa wa Morogoro.
Amesema,”Bodaboda unawahi wapi? Kwani ukiendesha taratibu hufiki, kwanini mnakiuka alama na michoro ya barabarani kwa makusudi? Kama riziki yako ipo ipo tu, Kuanzia leo nataka mbadilike na kuwa Bodaboda wa mfano”
Kwa upande wake Mkaguzi msaidizi wa Polisi, Saidi Maganga akitoa elimu kwa bodaboda wa kijiwe kilichopo mtaa wa Nyandile nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa, aliwataka kutambua umuhimu wa kuvaa kofia ngumu wao na abiria wanaowabeba huku Mkaguzi Kata wa Kata ya Ngerengere, Moses Mtikile akiwataka kutoa taarifa za wahalifu wanaofanya matukio ya wizi.