Kocha Msaidizi wa Simba SC, Juma Mgunda amesema wamekaa na kocha Mkuu, Roberto Robertinho, ili kufanya tathimini ya msimu uliomalizika Ijumaa (Juni 09) na kukabidhi mapendekezo yao kwa uongozi kuhakikisha wanalipa deni la mashabiki kwa msimu wa mashindano wa 2022/23.

Simba SC msimu huu haijatwaa taji lolote na iliishia hatua ya Robo Rainali kwenye michuano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mgunda amesema kabla ya kucheza mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Coastal Union, walikaa na Robertinho ili kufanya tathimini ya kikosi pamoja na wachezaji ambao wataendelea kusalia ndani ya timu kwa ajili ya msimu mpya.

Amesema msimu wa 2022/23 haukuwa na mafanikio kwao, kwani hawakufikia malengo yao licha ya wachezaji wao kufanya kazi nzuri uwanjani na kuifanya Simba SC kuwa timu inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga.

“Tumefanya tathimini ya timu hatukufanikiwa kufikia malengo yetu kwa asilimia 100, lakini tumeweza kufika nusu yake, tumeshakaa na Robertinho kuona wapi tulipokosea msimu huu, tunajipanga upya kwa msimu ujao ambao kwetu unadeni kubwa kwamashabiki wetu,” amesema Mgunda.

Amesema baada ya kukabidhi mapendekezo hayo ana imani uongozi utafanyia kazi kwa kuboresha kikosi cha timu yao kuelekea mashindano ya msimu ujao.

“Nina imani hakutakuwa na maboresho makubwa kwa sababu ya Simba SC ina wachezaji wazuri na tunaongeza wale ambao watakuja kushirikiana na watakaosalia kikosini kwa ajili ya msimu mpya wa 2022/23.” amesema Mgunda.

Kuhusu kiungo mshambuliaji wao, Saido Ntibazonkiza, Mgunda amesema ni mchezaji mzuri mwenye uwezo wa kusababisha na kuweza kufunga, jambo ambalo limeweza kumfanya kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania kiatu cha ufungaji bora.

“Ukiangalia msimu huu licha ya kushindwa kutwaa mataji lakini katika orodha ya ufungaji tumeweza kuongoza kuwa na idadi kubwa kuliko timu yoyote.

Hivyo hili ni deni kubwa kwetu kwa sababu tunatakiwa msimu wa 2023/24 kuhakikisha tunatwaa mataji hayo na kuendelea kuongoza katika ufungaji,” amesema kocha huyo anayedai msimu ujao wanakuja kivingine baada ya kufanya maboresho ya kikosi cha timu hiyo.

Kwa upande wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally amewataka mashabiki kuwatoyumbishwa na tetesi za usajili ambazo zinachochea migogoro baini yao na viongozi.

Amesema mashabiki na wanachama wanatakiwa kuwa makini na kutulia kwa tetesi watakazozipata, wanaandaa timu kubwa isiyofanana na ligi kuu Tanzania bali kikosi imara kinachokwenda kucheza michuano ya Super League.

“Kuna wachezaji tutaachana nao na kuwapa nafasi ya kwenda kutafuta changamoto zingine hasa kulingana mwaka huu tuna mashindano mengi, ikiwemo Super League,” amesema Ally

“Lazima tufanye usajili kulingana na mahitaji makubwa hatutaki kuingia na kuondolewa katika mchezo mmoja, lazima tufanye usajili mkubwa kulingana na ukubwa wa mashindano hayo, tunatoa fedha ya usajili kuleta wachezaji ambao watakuja kucheza michuano hiyo itakayoanza Agosti, lakini ndio hao hao watakaocheza na ligi,” amesema Ahmed.

Wakati huo huo Kiungo Mshambuliaji Saido Ntibazonkiza, amesema anafurahi kuona mashabiki wa Simba SC wakimuunga mkono katika kinyang’anyiro cha kuwania ufungaji bora jambo ambalo kwake anawashukuru wachezaji wenzake kwa sapoti kubwa.

Amesema anafurahi kuwa sehemu ya kuwania tuzo ya ufungaji bora na kumpongeza mshambuliaji wa Young Africans, Fiston Mayele kumpa changamoto hiyo na ana imani ni mchezaji mzuri.

“Kwa msimu ujao tutafanya vizuri nina Imani uongozi utakuwa tayari umeshakabidhiwa ripoti ya benchi la ufundi na kufanyia kazi kwa kufanya maboresho na msimu ujao tunatarajia kuwa imara,” amesema Saido.

Wizara ya Elimu yazifunga shule 900, sababu zatajwa
Simulizi: Dah! kumbe mdogo wangu anatembea na mke wangu