Wataalam wa Bodi ya maji Bonde la Wami/Ruvu, wamefanya ukaguzi wa matumizi ya maji kwenye maeneo mbalimbali, na kuifunga mifereji zaidi ya mitatu katika mto Lukulunge na Ngerenge, iliyokuwa ikichepusha na kupunguza kina cha maji.
Wataalam hao pia wamebaini uvunaji wa maji kwa kutumia ‘pump’ unaofanywa na askari wa kikosi cha jeshi la wananchi, na kutoa elimu ya usimamizi wa rasilimali za maji, ili iwe mfano kwa watumiaji wa maji.
Wakiwa kanda ya Ruvu chini, timu hiyo iliyokiambatana na Wataalam wa mamlaka ya maji Dawasa, pia wamebaini matumizi ya maji kinyume na sheria ya rasilimali za Maji, ya Mwaka 2009.
Uvunjaji huo wa sheria unatokana na kubaini uchepushwaji wa maji mto Ruvu, unaofanywa na mwekezaji wa mabwawa ya samaki, Eliona Koka wa kijiji cha Kisabi kata ya Muungano Kibaha, Pwani.
Mmiliki huyo, amekutwa akiendesha shughuli za ufugaji wa samaki katika vizimba huku akiwa hana vibali vya matumizi ya maji kutoka mtoni, jambo linalosababisha kuvunja sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji.
Lengo la ukaguzi huo, ni kufanya tathimini ya maji pamoja na kutoe elimu ya urasimishaji wa matumizi na utunzaji wa rasilimali za maji.