Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amemuagiza Mkandarasi anayejenga mradi wa maji wa Kibaoni katika Halmashauri ya Mpimbwe Mkoani Katavi kuongeza kasi na kufanya kazi mchana na usiku  ili kuwaondolea adha ya maji wananchi. 

Sanga ameyasema Mkoani Katavi na kuongeza kuwa hatua iliyofikiwa kwenye mradi inaweza kuwanufaisha Wananchi kupata huduma ya maji huku akiitaka RUWASA Wilaya ya Mlele kumsimamia Mkandarasi ili kuhakikisha Julai, mosi 2022 kuwafikishia huduma.

“Mradi unapofikia tu hatua ya kutoa maji zoezi la kwanza liwe ni kuwafikishia huduma wananchi, msisubiri hadi shughuli zote za mradi zikamilike ndipo mfungulie maji, sio busara kuacha wananchi wanateseka wakati kwa hatua iliyofikiwa ya mradi inawezekana wao kupata huduma,” amesema Mhandisi Sanga

Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Katibu Mkuu, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Gilbert Isaac alisema umelenga kunufaisha vitongoji vya Ndemanilwa, Kakuni, Ushirika na Isamvu na vitongoji vyote vya Kijiji cha Kibaoni.

Amesema mradi unatekelezwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya maradhi ya UVIKO-19.

Isaac amefafanua kuwa, mradi huo wa upanuzi unatumia kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 22,000 kwa saa na kwamba walikuwa wakitumia matenki mawili ya lita 90,000 ambayo anasema yalisababisha upungufu wa huduma.

“Baada ya kupata fedha kupitia mpango huu wa maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 tunafanya upanuzi na maboresha ya miundombinu ili kunufaisha kijiji chote cha Kibaoni,” aamefafanua Mhandisi Isaac

Hata hivyo, mradi huo unahusisha ujenzi wa tenki la ujazo wa lita 300,000 juu ya mnara wa mita 12 ikiwa ni tenki la zege, uchimbaji wa mitaro kilomita 11.2, ujenzi wa vituo 9 vya kuchotea maji Kibaoni, vituo 10 na chemba 32 katika Kijiji cha Inyonga.

Mradi wa Maji wa Kibaoni unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya Jemason Investment Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi 706,955,195.

G7 yakuna kichwa mfumuko wa bei Duniani
UN yataka waathirika dawa za kulevya watibiwe