Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema siku ya kimataifa ya usafirishaji haramu na kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa mwaka huu inaangazia athari za dawa hizo kiafya kwa Binadamu.

Kupitia ujumbe wake hii leo Juni 26, 2022 Katibu Mkuu amesema migogoro, majanga ya tabianchi, watu kulazimishwa kuhama makazi yao na umaskini uliokithiri vimetengeneza mazingira ya matumizi mabaya ya dawa za kulevya huku janga la UVIKO-19 likifanya hali kuwa mbaya zaidi.

“Watu wanaoishi katika hali za dharura za kibinadamu wana uwezekano mdogo sana wa kupata huduma na matibabu wanayohitaji na kustahili lakini vita na Uviko-19 vimesababisha madhara makubwa,” amesema Guterres.

Ameongeza kuwa, wahalifu wengi wamekuwa wakinufaika na hali hiyo kutokana na masaibu yanayowapata watu, huku akisema uzalishaji wa dawa aina ya ‘coceine’ upo katika kiwango cha juu zaidi.

“Kaatika hili pia imesababisha ongezeko la mara tano la kunaswa kwa madawa aina ya ‘methamphetamines’ na karibu ongezeko la mara nne ya kukamatwa kwa madawa aina ya ‘amfetamini’ katika muongo mmoja uliopita,” amefafanua Katibu Mkuu.

Aidha, amesema pamoja na kupata suluhisho la sera zisizo za kibaguzi zinazohusu watu, afya na haki za binadamu, unahitajika uungwaji wa mkono utakaoimarisha ushirikiano wa Kimataifa, ili kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya.

“Unahitajika uungwaji wa mkono utakaoimarisha ushirikiano wa Kimataifa, hii itasaidia kukomesha biashara haramu ya dawa za kulevya na kuwawajibisha wale wanaonufaika kutokana na taabu za binadamu wengine,” aliongeza Guterres.

Hata hivyo amesisitiza ulazima wa kuimarisha huduma za matibabu na usaidizi zinazotegemea sayansi kwa watumiaji wa dawa za kulevya, na kuwachukulia kama waathiriwa wanaohitaji matibabu badala ya adhabu.

“Katika hili, ubaguzi na unyanyapaa pamoja na matibabu kwa wale wanaoishi na magonjwa ya kuambukiza kama vile VVU/UKIMWI na homa ya ini hautakubalika na tutawachukulia hatua, hatuwezi kuruhusu tatizo la dawa za kulevya kuathiri zaidi maisha ya watu.” amesema.

Kuhusu siku hii ya kimataifa dhidi ya matumizi mabaya wa madawa ya kulevya na usafirishaji haramu, Guterres amesema watarejelea dhamira yao ya kukomesha tatizo hilo na kusaidia wale walioathiriwa ili kupunguza madhara zaidi.

Mkandarasi 'abanwa mbavu' mradi wa maji
DWJ yaanza rasmi 'maziko' ya kukata tamaa