Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Dodoma (DWJ), kimewarejesha masomoni wanafunzi wawili waliokata tamaa ya kuendelea na kidato cha tano, baada ya kushindwa kumudu gharama za mahitaji mbalimbali ya shule.

Mwenyekiti wa DWJ, Oliver Nyeriga ameyasema hayo jijini Dodoma na kusema, kwa kuwapa mahitaji Wanafunzi hao ili waweze kuendelea na masomo, ni mwanzo wa kuwashika mkono watoto wengine wenye uhitaji kama huo ili waweze kuendelea na masomo.

“Sisi wanawake ni wazazi, tunajua umuhimu wa elimu kwa watoto wetu hivyo hatutakubali kuona watoto wetu wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kukosa mahitaji,”amesema mwenyekiti huyo.

Akiongea katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka amewataka wanafunzi hao wakasome kwa Juhudi, ili kuwa mfano wa kuigwa na kuwaasa wasijiingize Kwenye makundi yasiyofaa.

“Mimi napenda sana Elimu na ni kipaumbele changu kwahiyo mnavyotoka hapa muende mkasome na tutakuwa tunafuatilia maendeleo yenu mkasome ili nanyi badae mkasaidie wengine” amesema Mtaka.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga amekipongeza Chama hicho cha Waandishi wa Habari wanawake Dodoma, kwa kuibua wanafunzi ambao ndoto zao za kuendelea na masomo zimepotea.

“Niwapongeze kwa hatua hii, lakini pia watoto wetu mkasome ili nanyi mkishafanikiwa mkasaidie wengine ambao watakuwa na mazingira kama haya ambayo mnayapitia ninyi sisi sote tumesoma kwa kusaidiwa” amesema Dkt. Mganga.

Wakitoa shukurani zao kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kwa Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake (DWJ), Wanafunzi Jumbe Mohamed na Ikram Said wamesema msaada huo umefanikisha azma yao za kurudi shuleni na kuahidi kusoma kwa bidii.

Jumbe Mohammed Jumbe mwenye ufaulu wa daraja la kwanza wa Mtihani wa kidato cha nne na kupangiwa Shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga Tech, na Ikram Said aliyepata daraja la kwanza na kupangiwa shule ya Sekondari Tosamaganga ya Mkoani Iringa, wamepatiwa msaada huo na utawawezesha kufikia ndoto zao za kimasomo walizojiwekea.

Katibu Tawala mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga akiwa na wanafunzi Jumbe M. Jumbe na Ikram Said pamoja na baadhi ya Waandishi wa Habari Wanawake wa DWJ, ofisini kwake jijini Dodoma.

UN yataka waathirika dawa za kulevya watibiwe
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Juni 26, 2022