Bomu la kujitoa muhanga limelipuka katika kituo cha polisi mashariki mwa Pakistan jioni Jumatano na kuuwa watu wasiopungua 9 na wengine 20 kujeruhiwa.
Hata hivyo hapakuwa na madai yoyote yaliyotolewa mara moja na kikundi chochote kwamba kimehusika na shambulio hilo karibu na Lahore, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Punjab.
Ofisa wa Polisi, Haidar Asraf amesema aliyejitoa muhanga alikusudia kuulipua msikiti katika mji wa wilaya ya Raiwind, ambako mkutano mkubwa wa kidini ulikuwa unafanyika.
Mkusanyiko huo ulikuwa umeandaliwa na taasisi ya Kiislam inayojulikana kama Tableeghi Jamaat au chama cha masheikh.
Usalama kwa kawaida umeimarishwa katika mtaa huo kwa ajili ya mkutano huo wa kidini wa kila mwaka.
Chama hicho cha kidini ni dhehebu kubwa la Kiislam ambalo linahubiri kuwa Waislam wafuate mwenendo wa Mtume Muhammad na kuwaambia wafuasi wao wanajukumu kusafiri kote ulimwenguni na kuutangaza Uislam.