Kocha msaidizi wa timu ya Simba, Masoud Djuma amesema watapambana mpaka tone la mwisho ili kufuzu hatua inayofuata ya michuano ya kombe la Shirikisho dhidi ya Al Masry.

Kocha huyo amesema hayo baada ya kikosi cha SImba kuwasili mapema hii leo mjini Port Said, tayari kwa mchezo huo utakaochezwa mwishoni mwa juma hili.

Masoud amesema hatua ya kucheza dhidi ya wapinzani wao katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es salaam, imewafanya  kugugundua mambo mengi likiwepo suala la mapungufu ambayo wameyafanyia kazi ili kuibuka kidedea.

Kocha huyo kutoka nchini Burundi ameongeza kuwa, hawawezi kukata tamaa licha ya kupata sare ya mabao mawili nyumbani lakini wataingia kwa tahadhari na kupunguza makosa yalijitokeza ili kupata matokeo chanya.

“Kuna dakika 90 nyingine tutazicheza hapa Misri na tunaweza kufanya vizuri kwa kuwa hata wao walifanya makosa tukapata mabao mawili,” alisema Masoud.

Simba imekuwa na historia nzuri inapokutana na timu zenye asili ya Kiarabu kitu ambacho kinawapa matumaini yakuwatupa nje Al Masry.

Jeshi la Polisi latoa ufafanuzi kuhusu mwili uliookotwa
Bomu lauwa watu 9 Pakistan