Msafara wa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika Wekundu Wa Msimbazi Simba mapema hii leo uliwasili salama mjini Port Said, tayari kwa mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya mtoano wa kombe la shirikisho barani Afrika.

Kikosi cha Simba sambamba na jopo la waamuzi kiliwasili mjini humo mishale ya saakumi na mbili asubihi kwa saa za Misri, sawa na saa moja asubuhi kwa saa za Afrika mashariki.

Kabla ya kuelekea mjini Port Said msafara wa Simba uliwasili Cairo Saa 7:50 usiku wa jana ikitokea Addis Ababa, Ethiopia ambako ilipitia kuunganisha ndege ikitokea Dar es Salaam, baada ya kuondoka jana jioni.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo, msafara wa Simba SC uliaanza safari iliyowachukua muda wa saa tatu kwa barabara kuelekea mji wa Port Said kwa basi maalum la kukodi.

Mkuu wa Msafara, James Mhagama ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kanda ya mikoa ya Njombe na Ruvuma, baada ya kuwasili hapa alimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Misri, Said Suleim Nassor pamoja na wenyeji wao, Al Masry kwa mapokezi mazuri.

Simba watakuwa ugenini dhidi ya Al Masry katika mchezo huo wa marudiano utakaochezwa Jumamosi Uwanja wa Port Said mjini Port Said, Misri ikihitaji ushindi wowote kusonga mbele, baada ya sare ya 2-2 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam Jumatano wiki iliyopita.

Msafara wa Simba upo chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’ na unaundwa na wachezaji 20, ambao ni makipa; Said Mohamed ‘Nduda’ na Aishi Manula.

Mabeki: Yussuf Mlipili, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Mganda Juuko Murushid, Mghana Asante Kwasi, Erasto Nyoni na Paul Bukaba.

Viungo: Mghana James Kotei, Said Ndemla, Muzamil Yassin, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto na Shiza Kichuya.

Washambuliaji: Mganda Emmanuel Okwi, Mrundi Laudit Mavugo, John Bocco, Mghana Nicholaus Gyan na Juma Luizio.

Kocha Mkuu, Mfaransa Pierre Lechantre, Msaidizi, Mrundi Masoud Juma, Kocha wa Mazoezi ya Nguvu, Mtunisia Mohammed Aymen Hbibi, kocha wa makipa, mzalendo Muharami Mohammed ‘Shilton’,  Dk. Yassin Gembe, Meneja Richard Robert na Mtunza Vifaa Yassin Mtambo.

Lwandamina ana uhakika dhidi ya Township Rollers
Nsato: Matukio ya uhalifu nchini yamepungua, jeshi liko imara