Mwamuzi Habib ‘Mkarafuu’ Mohammed aliyechezesha pambano la Karim ‘Mandonga’ Said na Salim Abeid lililounguruma Jumamosi (Septemba 24) mjini Mtwara amesimamishwa.
Mkarafuu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha waamuzi wa ngumi za Kulipwa nchini, ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa muda baada ya kukiri kushindwa kumudu kuchezesha pambano hilo.
Matokeo ya pambano hilo yalifutwa na Rais wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa baada ya mwamuzi kuonyesha kutolimudu baada ya Mandonga kupigwa na kudondoka chini lakini hakumhesabia kama kanuni zinavyotaka hadi aliponyanyuka.
Katibu wa Chama cha waamuzi wa ngumi za kulipwa, Emmanuel Mlundwa amesema mwamuzi huyo ametakiwa kurudi darasani kabla ya kuruhusiwa kuendelea na majukumu ulingoni.
Amesema rais wa TPBRC hakukosea kufuta matokeo kwa kuwa kama yangeingizwa kwenye rekodi, mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) ungehitaji video zake kwanza.
“Hivyo ingeleta mtizamo hasi kwenye ngumi zetu, lakini kama Chama tumejiridhisha kuwa kulikuwa na makosa mengi ya kiuamuzi kwenye pambano hilo, huenda yamechangiwa na waamuzi wetu kukaa muda mrefu bila kushiriki kwenye kozi mbalimbali na ndicho kimetokea kwa Mkarafuu,” amesema Mlundwa.
Amesema kutokana na makosa hayo, Chama kimemsimamisha mwamuzi huyo kuchezesha pambano lolote hadi atakaporudi darasani kuongeza ujuzi kwenye kozi za waamuzi miezi miwili ijayo,” amesema.
Mwamuzi huyo ameridhia adhabu hiyo na kukiri kushindwa kumudu pambano hilo ambalo alidai uamuzi wake ulitokana na makosa ya kibinadamu.