Uongozi wa Klabu ya Geita Gold FC uko kwenye wakati mgumu baada ya mshambuliaji Miraj Athuman ‘Sheva’ kugomea mazoezi kwa kile kinachodaiwa kutokamilishiwa fedha zake zote za usajili (signing fees) alizoahidiwa mwanzo.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai nyota huyo anadai kiasi cha Shilingi milioni 3 alizoahidiwa wakati akisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu, lakini hadi sasa ameshindwa kupewa kwa wakati kwani viongozi hao waliwekeza nguvu zaidi kwa kiungo wao mshambuliaji, Said Ntibazonkiza.

Taarifa hizo zimeongeza kuwa, Ntibazonkiza aliyejiunga nao siku chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa, akitokea Young Africans alitaka aingiziwe fedha zake zote za usajili walizokubaliana ndipo viongozi wakaamua kuachana kwanza na Sheva ili wakamilishe usajili wa Mshambuliaji huyo mzawa.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Klabu hiyo ya Mkoani Geita, Leonard Bugomola alishindwa kuweka wazi juu ya taarifa hizo, huku akisema kuna mambo madogo ambayo wao kama viongozi wanayashughulikia na kila kitu kitakuwa wazi.

Kwa upande wa Sheva hakutaka kulizungumzia hilo, huku akisema ameomba uongozi wake kwenda nyumbani kwa siku tatu ili kutatua changamoto za kifamilia.

Hata hivyo viongozi wa Geita wanapambana usiku na mchana ili kumpatia Mshambuliaji huyo fedha zake na kuepuka yaliyowakuta msimu uliopita baada ya kumsajili Ditram Nchimbi na kushindwa kumtumia kwa sababu kama hizo.

Bondia Mandonga amponza mwamuzi Mkarafuu
Ally Kamwe aomba ushirikiano Young Africans