Bondia mtanzania Hassan Mwakinyo aliyeibuka na ushindi baada ya kumchapa mpinzani wake raia wa Uingereza Sam Eggington katika pambano lililochezewa Birmingham amesema mpaka sasa amepokea mikataba mitatu kutoka sehemu tofauti tofauti ukiwemo mmoja kutoka kwa bondia Floyd Mayweather.
Bondia Mwakinyo amesema bado hajafanya uamuzi wa kusaini mikataba hiyo kwani anaamini kuwa Tanzania itamfanyia kitu kutokana na heshima kubwa aliyoileta hapa nchini ya kumkung’uta TKO bondia huyo wa Uingereza.
”Tumepokea simu kwa kambi ya TMT ya Mayweather anataka twende kwenye gym yake tukafanya naye kazi, lakini tumeshindwa kuyakubali yote hayo kwa sababu tunaamini Tanzania haijanishindwa bado, nina mikataba mitatau mpaka sasa ambayo sijafikia kuisaini na wala sijaamini kama naweza kusaini sababu siamini kama Tanzania inaweza ikashindwa kufanya chochote kwa ajili yangu, hayo yatakuja kama ntaona Tanzania imeshindwa kufanya kitu kwa ajili yangu” amesema Mwakinyo.
Pia Mwakinyo amewasilisha ombi lake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumtaka kutoa fursa katika michezo mbalimbali hapa nchini kwani wapo watanzania wenye vipaji lakini hawajulikani na hawajui namna ya kufikia ndoto zao.
Aidha amewataka watanzania kuwa na ushirikiano mkubwa kwani amelalamika kuwa watanzania wengi hawana ushirikiano ni watu wa kukatishana tamaa
”Tanzania tunashindwa kusapotiana wenyewe mchezaji anayeenda kucheza nchi za nje labda anacheza na Mayweather kwakuwa umeanza kumsikia Mayweather unahisi yeye ndiyo atashinda lakini ukweli ni kwamba hakuna bingwa anayefanya mazoezi kiasi kwamba akipigwa ngumi haiumi, hakuna ngumi ambayo haiumi kila ngumi inauama” amesema Mwakinyo.