Ni suala la muda tu kwa mshambuliaji wa Marumo Gallants ya nchini Afrika Kusini, Ranga Chivaviro kutua Young Africans ni baada ya kusaini mkataba wa awali wa miaka miwili ya kukipiga hapo huko nyota watatu wakitajwa kuondoka ili wampishe Mshambuliaji huyo.
Young Africans imepanga kukifanyia maboresho kikosi chao ili kifanye vema katika msimu ujao ambao wanakwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika sambamba na ndugu zao Simba SC.
Wapo baadhi ya wachezaji wanaotajwa kuja kujiunga na timu hiyo, kuelekea usajili mkubwa wa msimu ujao kati ya hao ni Chivaviro ambaye amezidiwa bao moja pekee na Fiston Mayele mwenye saba aliyetwaa ufungaji bora msimu huu.
Mmoja wa Mabosi wa Young Africans amesema Chivaviro amesaini mkataba wa awali wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo, ambaye anatarajiwa kutua nchini siku yoyote kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine za usajili.
Bosi huyo amesema kuwa mshambuliaji huyo anatarajiwa kuja kuchukua nafasi za wachezaji wawili watakaochwa na timu hiyo, ambao ni Tuisila Kisinda na Bernard Morrison anayetajwa kutimkia Singida Big Stars.
Ameongeza kuwa mshambuliaji huyo amekubali kujiunga na Yanga huku akiikataa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kutokana na dau nono ambalo amewekewa mchezaji huyo.
“Chivaviro anasubiria utambulisho pekee Young Africans, kwani tayari ameshasaini mkataba wa awali wa miaka miwili huku akisubiria kutambulishwa.
“Mkataba huo wa awali ni wa ajira bado huo wenyewe wa kuichezea Young Africans hadi dirisha la usajili litakapofunguliwa kuelekea msimu ujao ambao tumepanga kufanya vema.
“Chivaviro akija Young Africans mchezaji mmoja kati ya hawa wawili yaani Morrison na Kisinda mmoja wao atampisha ili achukue nafasi yake katika msimu ujao,” alisema bosi huyo. Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said alizungumzia hilo la usajili kwa kusema kuwa: “Usajili wetu wote unasimamiwa na kocha wetu Nabi (Nasreddine) ambaye anapendekeza mchezaji wa kusajiliwa na kuachwa.”