Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam imemhukumu aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mataka, kulipa faini ya Shilingi milioni nane au kutumikia kifungo cha miaka minne jela.
Mkurugenzi Mataka, amekutwa na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia hasara Serikali ya Shilingi Bilioni 71.
Uamuzi huo umetolewa leo, Agosti 20, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega wakati wa kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili hukumu.
Mbali na mshtakiwa Mataka, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu mstaafu, Dkt. Ramadhan Mlinga na aliyekuwa Mwanasheria wa PPRA , Bertha Soka, wamehukumiwa kulipa faini ya Shilingi Milioni 2, kila mmoja au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya katika shitaka moja la kughushi mhutasari wa kikao.
Dkt.Mlinga na Soka walidaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA Ilala, Dar es Salaam walighushi muhtasari wa kikao wa tarehe hiyo, wakionesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL ikodishe ndege aina ya Airbus, Mkataba ambao unadaiwa kuisababishia serikali hasara kubwa.