Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametangaza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, kilichotokea leo, saa tano kamili asubuhi.
Rais Mwinyi ameeleza kwa masikitiko kuwa Maalim Seif amefariki akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu.
“Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif amefariki dunia. Maalim amefariki wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambako alikuwa amelazwa tangu tarehe 9, Februari mwaka huu,” amesema Dkt. Mwinyi.
Rais Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo kufuatia msiba huo wa kitaifa.
Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amemlilia kiongozi huyo, akiandika ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Mwinyi, Familia, Wazanzibari, wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania wote. Mungu amweke mahali pema peponi. Amina,” ametweet Rais Magufuli.