Baada ya kuwa na mazingira magumu ya kutimiziwa ahadi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, mshambuliaji kinda wa klabu ya Arsenal Chuba Amechi Akpom, ameonyesha kuwa tayari kucheza soka lake kwenye ligi daraja la kwanza nchini England.
Akpom yu tayari kushuka hadi ligi daraja la kwanza nchini England, kufuatia klabu za Brentford, Cardiff City na Fulham kuonyesha nia ya kumsajili katika dirisha dogo la usajili.
Tayari Arsenal wameonyesha nia ya kumuachia mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, lakini kwa sharti la usajili wa mkopo.
Arsenal wameweka sharti hilo, kwa lengo la kutaka kuendelea kumtumia Akpom kwa mipango yao ya baadae, na wanaamini kama atafanikiwa kuondoka katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, atapata nafasi ya kujiendeleza ili kutunza uwezo wake kisoka.
Akpom amekuzwa na kuendelezwa kisoka na klabu ya Arsenal tangu akiwa na umri mdogo, na kwa mara ya kwanza alionekana katika kikosi cha wakubwa mwaka 2013.