Kiungo wa zamani wa majogoo wa jiji (Liverpool) Mohamed Sissoko anajipanga kurejea katika ligi ya nchini England.

Sissoko ameweka dhamira hiyo baada ya kumaliza mkataba wake na klabu ya Pune City inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini India, na tayari ameshaanza kufanya mazoezi na kikosi cha West Bromwich Albion.

Hatua hiyo inaaminika huenda ikamsaidia kufikia lengo la kucheza tena katika ligi ya nchini England, akiwa na klabu ya West Brom yenye maskani yake The Hawthorns, katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Kiungo huyo ambaye aliwahi kucheza soka akiwa na klabu za Juventus (Italia), PSG (Ufaransa) na Valencia (Hispania) ameliambia gazeti la Mirror Sport: “Bado nina njaa ya kucheza soka. Na ndio maana ninataka kurejea barani Ulaya. Kufikia umri wa miaka 31 sio sababu ya kuacha kucheza soka. Labla ikitokea nimekufa!

“Nimepanga kucheza soka kama alivyofanya Alessandro Del Piero, alicheza akiwa na umri wa miaka 40. Na wapo wachezaji wengi ambao wamefikisha umri zaidi ya miaka 30 lakini wanasaini mikataba mipya na wanacheza. Hivyo umri si lolote, si chochote.

“Unatakia kuwa na utimamu wa mwili na kujituma wakati wote kwa ajili ya kuisaidia timu yako kufikia malengo. Kama utafanya hivyo hakuna atakaeweza kukupinga ama kukuweka benchi kwa kigezo cha kuangalia umri.

“Naipenda England. Nimewahi kuwa hapa kwa mafanikio makubwa. Ninaipenda ligi ya hapa, ninapenda ushindani uliopo katika ligi ya hapa. Kwa ufupi ninapendezwa na kila kitu cha nchi hii kinachohusiana na soka. Ndio maana nimeamua kurudi.”

Brentford, Cardiff City, Fulham Zapigana Vikumbo Emirates Stadium
Tanzania Yashindwa Kusogea Viwango Vya Ubora Duniani