Kiungo wa kati wa Timu ya Taifa ya Ureno, Bruno Fernandes, ametajwa kuwa ndiye nahodha mpya wa kikosi cha Manchester United kuelekea msimu mpya 2023/24.
Klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England imetangaza Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 atachukua nafasi ya beki, Harry Maguire, ambaye alivuliwa unahodha wa timu na Kocha, Erik ten Hag, baada ya nyota huyo wa kimataifa wa England kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.
Fernandes ana mabao 64 na asisti 54 katika michezo 185 kwa klabu hiyo katika michuano yote, na msimu uliopita alitumia muda mwingi wa kiongoza timu wakati Maguire akiwa benchi au kuumia.
ESPN iliripoti Mei 31, mwaka huu United iko tayari kusikiliza ofa kwa Maguire msimu huu wa joto na kutarajia nia kutoka kwa West Ham, ambao walifanya uchunguzi kuhusu kupatikana wake wakati wa dirisha la usajili la Januari iliyopita.
“Kiungo huyo wa Ureno tayari ameshavaa kitambaa cha unahodha wa United mara nyingi na Ten Hag amethibitisha sasa ataiongoza timu hiyo kwa misingi ya kudumu,” ilisema taarifa ya United.
“Kama nahodha, mshindi huyo mara mbili wa tuzo ya Sir Matt Busby kama Mchezaji Bora wa mwaka wa klabu, ataendelea kuiongoza United ikipigania mafanikio katika msimu wa 2023-24.”
Fernandes alikosolewa kwa uchezaji wake duni wakati United wakichezea kichapo cha mabao 7-0 kutoka kwa wapinzani wao Liverpool hapo Machi, mwaka huu.
Kampeni ya United ya kujiandaa na msimu mpya inaendelea, na kikosi hicho cha Old Trafford kiliifunga Lyon ya Ligi Kuu Ufaransa bao 1-0, mechi iliyochezwa Jumatano juma hili.
Baadae United ilisafiri hadi Marekani, ambapo itamenyana na Arsenal, Wrexham, Real Madrid na Borussia Dortmund katika mechi za kirafiki kabla ya kuanza kwa msimu mpya.