Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando imezindua rasmi huduma ya Kisasa ya upasuaji kupitia matundu Madogo, (Minimally Invasive Surgeries).
Uzinduzi wa huduma hiyo imefanyika hii leo Ijumaa Julai 15, 2022 ukihudhuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando Dkt. Fabian Masaga ameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya MOI kwa kuwasaidia madaktari wa Bugando kuwajengea uwezo wa hospitali hiyo kufanya upasuaji kwa kutumia matundu madogo.
Amesema, kabla ya huduma hiyo Madaktari walihitaji kufungua kidonda cha majeruhi ili kufanya matibabu kwenye magoti, lakini kwasasa wataingia sehemu za ndani za maungio na kutibu haraka na kwamba tayari wagonjwa 18 wamefanyiwa upasuaji.
“Mkuu wa mpaka leo hii zaidi ya wagonjwa 18 wamefanyiwa upasuaji kwa njia ya kutumia matundu madogo kwa kushirikiana na Madaktari na wauguzi kutoka Muhimbili na MOI na Idara zaidi ya tano zitakuwa zinatoa huduma za upasuaji kwa njia ya matundu madogo” amesema Dkt. Masaga.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewapongeza Viongozi na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando kwa kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi wa kanda ya ziwa ambazo zimekua zikiboreshwa siku hadi siku.
Amesema, wananchi wa kanda ya ziwa wapotao takribani milioni 14 hivi sasa wanapata huduma bora na za kisasa kabisa katika hospitali hiyo huku akizitaja huzuma za magonjwa ya Uzazi Na vizazi, njia ya mfumo wa mkojo, ubongo na upasuaji wa jumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru amesema nia ya Serikali kuleta huduma za kibingwa nchini katika sehemu tofauti in alengo la kuwasaidia wananchi kupata huduma hizo ndani.
Amesema, wananchi wengi hawana uwezo wa kifedha kwenda kupata matibabu nje ya nchi na kwamba kwa kutumia wataalamu wa ndani kupeana mafunzo haya itasaidia Madaktari kueneza huduma za kibobezi nchini Tanzania.