Uongozi wa Young Africans kupitia kwa Afisa habari wa klabu hiyo Hassan Bumbuli amesema kuwa hawajakubaliana na adhabu iliyotolewa na kamati ya maadili ya TFF kwa Makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Lugano Mwakalebela.
Kamati ya Madili kupitia TFF ilitangaza adhabu ya kumfungia katibu mkuu huyo wa zamani wa Shirikisho hilo, Ijumaa (April 02), baada ya kujiridhisha Mwakalebela alikuwa na makosa ya kimaadili alipozungumza na waandishi wa habari mapema mwaka huu.
Bumbuli amedai kuwa Young Africans imeshangazwa na suala hilo kuwa la binafsi na kufungiwa Mwakalebela wakati kilichopelekea afungiwe ilikuwa ni uamuzi wa klabu na si wa Mwakalebela.
“Tumechelewa kukata rufaa kwa kuwa tulikuwa tunasubiri muongozo wa TFF, lakini kama klabu hatujakubaliana na adhabu hiyo kwa makamu mwenyekiti wetu,” amesema Bumbuli.
“Mwakalebela alizungumza kile kilichoamuliwa na klabu, na hadi anakizungumza ilikuwa ni uamuzi wa klabu, lakini ameadhibiwa kama Mwakalebela.
“Klabu hatujakubaliana na adhabu hiyo na wakati wowote kuanzia sasa tutawasilisha rufaa kupinga adhabu aliyopewa makamu mwenyekiti wa klabu yetu,” amesema Bumbuli.
Amesema wakati wowote kuanzia sasa Uongozi wa klabu hiyo itawasilisha rufaa kupinga adhabu ya kufungiwa miaka 5 na faini ya milioni 7 aliyopewa Mwakalebela.