Bundi, ndege ambaye ni nadra kumuona mchana na mwenye sifa za aina yake kulingana na imani ya msimuliaji, leo amekuwa wa kwanza kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Bungeni, Maafisa wa Bunge walioingia awali kwa lengo la kukagua ukumbi huo kabla ya kuanza kwa vikao vya Mkutano wa Bunge walimuona bundi hiyo akiwa anajiachia juu ya dari.
Watumishi hao walifanya jitihada za kumuondoa, lakini alikuwa akihama kutoka eneo moja hadi lingine. Maafisa hao waliohangaika na bundi huyo hawakufanikiwa kumuondoa kama walivyotaka.
Hata hivyo, baada ya muda, imeelezwa kuwa ndege huyo hakuonekana tena na haijulikani aliondoka vipi ndani ya ukumbi huo.
Aidha, wakati wa kuanza kwa mkutano wa Bunge, Spika Ndugai alizungumzia mkasa huo akiwatoa hofu maafisa wa Bunge pamoja na wabunge kuwa hilo ni jambo la kawaida ndani ya jiji hilo.
“Waheshimiwa wabunge, asubuhi tumeanza kumuona bundi ndani ya jengo hili. Lakini kwa Dodoma, Bundi wa mchana hana madhara kwa hiyo ni mambo ya kawaida kabisa,” alisema Spika Ndugai.