Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amekiri kwamba haungwi mkono vya kutosha kuupitisha mpango wake wa Brexit, ambapo Wabunge wamepania kuunga mkono njia mbadala ili kuondoa msuguano katika mchakato huo.
Amesema kuwa kuna idadi ndogo sana ya wabunge wanaounga mkono mpango wake juu ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ambao umeshakataliwa mara mbili na wabunge hao.
Aliyasema hayo jana jioni alipokuwa akiwahutubia wabunge wa bunge la nchi hiyo ili kuwapa taarifa juu ya mazungumzo yake na viongozi wa Umoja wa Ulaya wiki iliyopita, ambapo amesema anamatumaini makubwa kwamba hali inaweza kubadilika wiki ijayo.
Aidha, mpango wa waziri mkuu huyo juu ya kujiondoa Umoja wa Ulaya unapaswa kupitishwa na wabunge wa bunge la nchi hiyo wiki hii ili Uingereza iweze kuondoka kutoka kwenye Umoja huo.
Waziri mkuu May bado anaendelea na juhudi za kujaribu kuwashawishi wabunge wauunge mkono mpango wake, ambapo amesema ni muhimu kwa bunge la nchi yake kuyazingatia matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika mnamo mwaka 2016 badala ya kutafakari wazo la kufanyika kura nyingine ya maoni juu ya Brexit.
Kwa upande wake kiongozi wa kikuu cha upinzani nchini humo, cha Labour, Jeremy Corbyn amesema kuwa kwasasa wakati umefika kwa bunge kuudhibiti mchakato wa Brexit, huku akisema serikali ya May inaushughulikia mchakato wa Brexit kwa njia ya kufedhehesha.
Hata hivyo, Umoja wa Ulaya unaendelea kujitayarisha ili kuikabili hali, endapo Uingereza itaamua kujiondoa kutoka kwenye Umoja huo bila ya mkataba, ambapo msemaji wa Umoja huo, Margaritis Schinas ameeleza kwamba uwezekano wa Uingezera kuondoka bila ya mkataba unazidi kuwa mkubwa.