Vyombo vya Habari nchini, sasa vipo huru katika kutafuta, kuhariri na kuchapisha au kutangaza habari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa haki yao ya kikatiba (Ibara ya 18, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977).
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kupitia tarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Innocent Mungy.
Hatua hiyo inafuatia Bunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambao ndani yake una sheria nane, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 iliyokuwa ikipigiwa kelele na wadau wa Habari waliokuwa wakitaka kubadilishwa kwa baadhi ya vifungu.
Mapendekezo.
Akisoma muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali -AG, Eliezer Feleshi alisema kifungu cha 5 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 kinapendekeza kufanya marekebisho kwa lengo la kumwondolea jukumu la uratibu wa matangazo yote ya Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Habari.
Alisema, marekebisho hayo yataiipa uhuru Serikali kuchagua chombo cha Habari kwa ajili ya matangazo yake kwa kuzingatia nguvu ya ushindani katika soko na kupendekeza kukifanyia marekebisho kifungu cha 38 kwa madhumuni ya kuongeza haki na uhuru wa maoni.
Alisema, “Muswada unapendekeza marekebisho ya vifungu vya 50, 51, 53, 54, 55, 63 na 64 kwa madhumuni ya kuweka adhabu tahafifu kwa makosa yatokanayo na ukiukwaji wa sheria hii.”
Aidha, kupitia tarifa hiyo, imeeleza kuwa, pia hatua hiyo ni utekelezaji wa haki za kimataifa za uhuru wa habari (kwa mujibu wa Tamko la Haki za Binadamu, 1948, Mkataba wa Kimataifa Kuhusu Haki za Kisiasa na Kiraia, 1966 na Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Binadamu.
Pongezi.
Aidha, Serikali pia imesema inawapongeza wadau wote walioshiriki kuchangia mawazo na mapendekezo ya kuifanyia mabadiliko hadi kupitishwa kwa Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 pamoja na marekebisho yake kama yalivyopitishwa na Bunge.
Akizungumza baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha mabadiliko hayo ya Sheria, Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amevipongeza vyombo vya Habari na Taassisi za Vyombo vya Habari nchini pamoja na wadau wa Jumuia ya Kimataifa kwa mchango wao wa mawazo na mapendekezo yaliyopelekea mabadiliko hayo muhimu kupitishwa na
Bunge.
Ushauri wa Waziri Nape.
Hata hivyo, Waziri Nape ameshauri Taasisi za Jumuia ya Kimataifa zinazopima Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani, kutumia taarifa za sasa badala ya zile za zamani ambazo zimekuwa zikionesha Tanzania iko nyuma katika suala zima la Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani.
“Wadau walileta mapendekezo 21 ambayo walitaka tuyapitie kwa pamoja, katika mapendekezo hayo, yakagawanyika katika makundi manne, hoja ambazo tulikubaliana baada ya majadiliano kwamba zibaki kama zilivyo kwenye sheria,” alisema Waziri Nape.
Aidha aliongeza kuwa, “kutokana na marekebisho yaliyofanyika katika Sheria hii, kuna mambo muhimu ambayo yanakuza uhuru na kuimarisha weledi katika Sekta ya Habari hapa nchini, ikiwemo kuifanya taaluma ya habari kutambulika kisheria kama zilivyo taaluma nyingine.”
Mengine ni kupunguzwa kwa adhabu na kuondolewa kwa makosa yanayohusiana na kashfa za kijinai, kupunguza mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, kuondoa adhabu kwa wamiliki wa mitambo ya uchapishaji, kuanishwa vyema kwa haki na wajibu wa wanahabari nchini.
Pia itaundwa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari (kifungu cha 11-18), kuundwa kwa Baraza Huru la Habari (Kifungu cha 24-34), kuanzishwa kwa Mfuko wa mafunzo wa wanahabari (Kifungui cha 22-23), kuwepo kwa Bima kwa wanahabri na masuala ya hifadhi ya Mifu ya jamii. (Kifungu cha 62) na Uhuru wa kumiliki vyombo vya habari nchini (Kifungu cha 6).
“Kwa kuzingatia masuala muhimu na mazuri yaliyopo kwenye Sheria hii baada ya kufanya marekebisho, Nape Moses Nnauye amewahakikishia wadau wa habari kuwa Serikali sasa itahakikisha vyombo vilivyoundwa katika Sheria hii vinatekeleza majukumu yake kikamilifu na haki za wanahabari zinasimamiwa ipasavyo na kutimiza wajibu wao,” ilieleza taarifa hiyo.