Mwili wa aliyekuwa rais wa Burundi hayati Pierre Nkurunziza unazikwa leo Juni 26, 2020 kwenye makaburi ya mji wa Gitega, mji mkuu wa kisiasa ulioko katikati mwa nchi hiyo.
Kwa mjibu wa tangazo lililotolewa na serikali ya Burundi, hafla itaanzia ‘Hospital du Cenquantenaire Twese Turashoboye’ iliyoko kwenye mkoa wa Karusi ambako maiti yake imehifadhiwa.
Hafla ya maziko inatarajiwa kuongozwa na Rais mpya Jenerali Evariste Ndayishimiye na wakuu wengine wa serikali.
Hayati Nkurunziza alifariki dunia tarehe 8 mwezi huu 2020, miezi miwili kabla ya kukabidhi madaraka kwa mrithi wake kufuatia uchaguzi uliofanyika mwezi wa tano.
Mlolongo wa magari yatakayosindikiza maiti yake utatoka kwenye hospitali hiyo na kuelekea katika mji wa Gitega ambao ni mji mkuu wa kisiasa ambapo wananchi wameombwa kusimama kwenye barabara kumuaga marehemu.
Hata hivyo kunatarajiwa hafla fupi ya jeshi kumtolea heshima za mwisho kwenye uwanja wa mpira wa Ingoma mjini Gitega, kabla ya mwili wake kupitishwa mbele ya wananchi watakaokuwa uwanjani humo kumwaga na baadaye kufanyika maziko rasmi.
Tangazo la serikali ya Burundi linasema kwamba shughuli nyingine, kama kuweka mashada ya maua kwenye kaburi lake au hotuba zitakazotolewa zitafahamika leo.
Ikumbukwe Nkurunziza alifariki dunia tarehe 8 mwezi huu kutokana na mshtuko wa moyo kama ilivyotangazwa na serikali ya nchi hiyo.