Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amesema wameandika barua kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro kuomba ulinzi kwa ajili ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu ili aweze kurudi nchini.

Mnyika amesema hayo leo Juni 25, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema barua hiyo wameiandika tangu mwaka jana na hawajajibiwa.

“Desemba 23, 2019 nilimuandikia barua rasmi IGP kuomba ulinzi wa polisi kwa ajili ya Makamu Mwenyekiti wa bara wa chama ambaye amekuwa akiishi nje kwa matibabu aweze kurudi, lakini mpaka leo hatujapatiwa majibu,” amesema Mnyika

Aidha, Mnyika amesema kama jeshi la polisi lina ushahidi wanayosema kuhusu tukio la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wautoe.

Alisema katika tukio la kushambuliwa Mbowe Dodoma, jeshi la polisi limejaribu kuonyesha kama vile hakushambuliwa na kwenda mbali zaidi kwa kudai wanakusudia kumpeleka mahakamani.

Aidha, amesema wakati muafaka ukifika wao kama Chadema watawaongoza wananchi kuhusu uchaguzi ujao na watazilinda kura zao kuhakikisha kwamba haki inatendeka na mabadiliko yanatokea

Simba, Young Africans zatakiwa kufuata nyayo za KMC FC
Maambukizi ya Covid 19 yafikia milioni 9.3 duniani