Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Seleman Matola, amesema wachezaji Rally Bwalya, Clatous Chama, Sadio Kanoute na Bernard Morrison wana kazi kubwa ya kufanya, katika kipindi hiki cha kupambania ubingwa wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.
Kazi kubwa kwa wachezaji hao wa kigeni ni kurekebisha makosa ya majukumu yao uwanjani ya kupiga mipira iliyokufa, ambayo ni sehemu ya kusaka ushindi kwa timu ya Simba SC.
Matola amesema kuwa tatizo la kushindwa kupata matokeo mazuri lina maumivu makubwa na wamegundua tatizo lilipo ikiwa ni pamoja na kushindwa kutumia mipira ya kona na faulo.
“Kushindwa kupata matokeo mazuri kwa Simba ni maumivu lakini tumegundua kwamba suala la kukosa kutumia mapigo huru, hilo nalo ni kosa, hivyo kwa wapigaji wa kona na faulo wote tutazungumza nao ili kuboresha makosa yetu.”
“Ikiwa kwenye mechi tunapata kona zaidi ya 9 na hazileti mabao, hilo ni jambo la kufanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi, bado tupo imara na makosa kila siku tunayafanyia kazi na tutazungumza na wachezaji wetu ili tuweze kupata ushindi pia kupitia mapigo hayo.
“Mfano kwenye mchezo dhidi ya Prisons tulipata kona tatu ziliweza kuwa na hatari kwenye lango la mpinzani lakini hatukufunga, bado kuna mechi zinakuja tunaamini tutafanya vizuri,” alisema Matola.
Simba SC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 31, huku ikianza vizuri Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga ASEC Mimosas ya Ivory Coast mabao 3-1.