Mshambuliaji kutoka DR Congo na klabu ya Al Ahly ya Misri Walter Binene Sabwa Bwalya, amesema kitendo cha timu yake kupangwa kundi moja na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kitamuewezesha kulipa kisasi cha msimu wa 2018/19, alipokua na Nkana FC ya Zambia.
Bwalya amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu matarajio yake kuelekea kwenye michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku akikumbuka namna Simba ilivyoizamisha Nkana FC kwenye mzunguuko wa kwanza wa michuano hiyo mwaka 2018 kwa kuifunga jumla ya mabao manne kwa matatu.
Amesema aliumizwa sana kwa wakati ule kufungwa na Simba SC tena kwa idadi kubwa ya mabao, na alikua anasubiri kwa hamu kubwa kukutanishwa tena na mabingwa hao wa Tanzania Bara.
“Nimekuwa furaha kwa sababu napata fursa nyingine ya kuweza kulipiza kisasi dhidi ya Simba SC ambayo iliniachia kumbukumbu mbaya wakati nikiwa Nkana FC, naamini nitautumia mchezo huo kwa kuhakikisha tunashinda michezo yote miwili.”
Kuhusu ‘Kundi A” ambalo michezo yake itaanza rasmi leo Ijumaa (Februari 12), Bwalya amesema kundi hilo ni gumu kutokana na timu zote kuwa na uzoefu wa michuano ya kimataifa.
“Kundi letu siyo rahisi kwa sababu timu zilizokuwepo zote ni ngumu na zimekuwa na uzoefu wa mashindano ambayo tunashiriki kwa muda mrefu, ukiwaangalia, AS Vita, El Merreikh na hata Simba hivyo lazima maandalizi yawe ya kutosha.
Mchezo wa kwanza wa ‘Kundi A’ unatarajiwa kucheza hii leo mjini Kinshasa, DR Congo kwa wenyeji AS Vita Club kuwakaribisha mabingwa wa soka kutoka Tanzania Simba SC.