Aliyewahi kuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungala ‘Bwege’ amesema wataendelea kuwa wapinzani endapo Chama cha Mapinduzi – CCM, kitashindwa kutekeleza sera na hakitajirekebisha katika utendaji wake wa kuwahudumia Watanzania katika misingi ya haki, uhuru na kuwapatia Maendeleo.
Bungala ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media Nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa wao kama Wanasiasa, wana wajibu wa kuikosoa Serikali kwa yale ambayo wanaona yana ulazima wa kutekelezwa kwa maslahi ya Taifa.
Amesema, “watu wakipata haki, uhuru upo, maendeleo yapo sasa hapo unakuwa mpinzani wa nini sasa, lakini wasipotekeleza, upinzani hautaisha kuna baadhi ya mambo yanatafakarisha mfano mimi nilitoka CCM kwa sababu ya kulazimishwa kulima muhogo, kipindi hicho mie Balozi nilikataa.”
Hata hivyo Bwege amesema “hilo tu lilinifanya nihame chama, unalazimishaje mimi nilime mihogo halafu nisimamie tena wananchi nao walime zao hilo kwa nguvu, sikupendezwa maana wamakonde wanasema sisi ni watoa taarifa hivyo nikalazimika kutoa taarifa na baadaye nilikamatwa, ila nilipinga.”