Tanzania inatarajiwa kujitangaza kimataifa kupitia Mkutano wa 28 (COP 28) wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, utakaofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia Novemba
28 hadi 12 Disemba 2023.

Hayo yamesemwa hii leo Novemba 11, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo wakati akitoa tamko kuhusu ushiriki na msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya mkutano huo.

Amesema, Tanzania imepanga kuendesha mkutano mkubwa wa pembezoni utakaowaleta pamoja wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na mabara mengine pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kuvutia wawekezaji katika fursa za mabadiliko ya tabianchi zilizopo nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo.

“Mkutano huu unalenga kuongeza chachu ya uwekezaji wa kimataifa kwa kutumia fursa katika sekta kwa kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani kote ili kufahamu fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania na mkutano huu utaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jafo.

Hata hivy, Waziri Jafo amesema katika kuwezesha ushiriki wenye tija, Tanzania imeandaa msimamo wa nchi kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya taifa katika majadiliano ambao umeandaliwa kwa kuzingatia sera, mipango na mikakati ya taifa na ushirikiano na makundi ya nchi.

Watoto 1,877,484 kuandikishwa elimu ya awali
Bwege: Kwa jambo hili tutaendelea kuwa Wapinzani