Mkuu wa Waamuzi wanaochezesha Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2021’ Essam Abdel-Fatah, amefichua kuwa Mwamuzi Janny Sikazwe kutoka Zambia alijihisi vibaya kiafya (KIHARUSI CHA JOTO) akiwa kwenye majukumu ya kuchezesha mchezo wa ‘Kundi F’ kati ya Tunisia dhidi ya Mali na kusababisha kupoteza umakini.
Ufafanuzi huo umetolewa kufuatia sintofahamu iliyojitokeza, kufuatia tukio la Mwamuzi huyo kumaliza mchezo huo kabla ya kutimia kwa dakika 90, huku Mali wakiongoza bao 1-0.
Essam Abdel-Fatah amesema Mwamuzi Sikazwe, alikumbwa na tatizo la Kiharusi cha joto, ambalo husababishwa na joto kali juu ya mwili wa Binadamu.
Dakika ya 79:43 Mwamuzi huyo alimwambia msaidizi wake wa akiba aongeze dakika 5, akimaanisha kuwa 90 zimekamilika lakini ilikua tofauti na muda aliokua akiudhania.
Cha ajabu ilipofika dakika ya 85 akapuliza kipyenga kumalizika kwa dakika 90 za mchezo huo na kuzua taharuki kwa maafisa wa benchi la ufundi la Tunisia.
Ikatokea kubishana na akaanzisha upya mchezo kwa kuudunda, lakini ilipofika dakika ya 89:23 akapuliza kipyenga kumalizika mchezo, hatua ambayo iliendelea kupingwa na maafisa wa benchi la ufundi la Tunisia.