Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeipa ushindi klabu ya Al Ahly Tripoli ya Libya, kufuatia klabu ya Biashara United Mara kushindwa kwenda mjini Benghazi, kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili wa Kombe la Shirikisho hatua ya Kwanza.
Shirikisho la soka nchini ‘TFF’ limethibitisha maamuzi ya kamati hiyo ya ‘CAF’ leo Jumatano (Novemba 03) majira ya mchana, kwa kuweka taarifa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Kamati ya Mashindano ya ‘CAF’ imejiridhisha kuwa Biashara United Mara hawakuwa na sababu zenye mashiko kukwama kwenda Libya kucheza mchezo wa mkondo wa pili, ambao ulipangwa kuunguruma Oktoba 23.