Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Rajab Kahali maarufu Harmonize ametangaza rasmi kutozitambua tuzo zinazoendelea hasa alizotajwa kama mmoja wa wasanii wenye kuwania tuzo hizo mwaka huu.

Harmonize ameutumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kuandika ujumbe kupitia Insta story yake, wenye kumaanisha kuwa kwa sasa hayuko tayari kuwasumbua mashabiki wake kuhangaika kumpigia kura kwa kuwa yeye mwenyewe hayuko tayari na mapokezi ya tuzo hizo.

“Sijateuliwa kuwania tuzo yeyote kwa hivyo tafadhali usipoteze kifurushi chako cha Internet kunipigia kura, hii ni kwa wanachama wa Konde Gang pekee” ameandika Harmonize.

Msanii huyo ambaye kwa sasa yuko nchini Marekani kwa ziara yake ya kikazi ameyasema hayo muda mfupi baada ya kutangazwa kwa majina ya wasanii walioteuliwa kuwania tuzo za African Entertainment Awards USA ambazo msanii huyo ameteuliwa kwenye vipengele kadhaa ikiwamo cha msanii bora wa kiume Mashariki, Kusini na Kaskazini mwa Afrika (Best Male Artist – East/South/North Africa).

Kitendo hicho kimeibua sintofahamu kwa mashabiki wa Harmonize kwenye mitandao ya kijamii, huku wengi wakijadili kuwa pengine kujiengua kwa msanii huyo kumekuja kufuatia kutopangwa kwake kwenye vipengele kama msanii bora wa kiume, msanii bora wa mwaka nk, vipengele ambavyo vimeshikiliwa na wasanii kama Burna Boy, Davido, Wizkid, Facolistic, Shatta Wale, Stone bwoy, Diamond Platnumz na wengine kadhaa ambao wanatajwa kuwa pengine wana hadhi moja na msanii huyo kwenye kiwanda cha muziki barani Afrika.

Ukiachana na sakata la Harmonize, Vuguvugu lingine kutoka kwa mashabiki na wadau kadhaa wa mzuki limezuka muda mfupi baada ya mtandao maalumu wa waandaji wa tuzo hizo kuweka orodha ya wasanii wenye kuwania tuzo, ikiwa imeambatana ana  jina la msanii Mac Voice ambaye mwezi mmoja tu, uliopita alitambulishwa rasmi kuingia kwenye tasnia ya muziki akiwa chini ya msanii Rayvvany kupitia Next Level Music.

Baadhi ya watu wameiponda hatua ya waandaaji wa tuzo hizo kulipitisha jina la msanii huyo kutokana na kuwa ni muda mfupi sana tangu ameanza muziki hivyo pengine kuna vigezo havijazingatiwa katika mchakato huo huku wengine wakidai kuwa inawezekana kuna mchezo usio sawa unaochezwa bila mashabiki kufahamu kwa lengo la kugushi ili kumpandisha msanii huyo.

Kupitia kwenye ukurasa wa mtandao wa Instagram wa mchambuzi wa maswala ya muziki maarufu kwa jina la Advocate Fi ameingilia kati swala hili kwa kuandika na wazi mtazamo wake juu ya kinachoendelea.

“Tuzo za michongo zinazokuza Wasanii wetu mabroila. Msanii anasikika leo alafu mwisho wa mwezi anakuwa nominated kwenye international awards haha. Nadhani njia hizi hazikuzi Wasanii wetu na inafundisha somo baya kwa upcoming Artists na kuharibu mindsets zao.

Lava Lava, Ibrah wote wamepitia kwenye pattern hiyo ya kuku broila na kuaminishwa ukubwa ambao hawana ndomana utaona graph zao zimestuck mahali no more, no less.

Kwa Msanii kukomaa inahitaji miaka isiyopungua 7 mpaka 10. Take it or leave it otherwise tutaendelea kukuza mabroila kwenye industry. Fans base aliyonayo Alikiba, Diamond haikuzaliwa ndani ya mwezi mmoja sababu walikuwa na Usimamizi unaojitambua kwa wakati huo.

Simply, Views, streams, insta followers, Amapiano, kiki na tuzo za michongo ni viungo vinavyopika na kuivisha Wasanii broila kwenye Bongo Industry”. ameandika Advocate Fi kwenye mtandao wake wa instagram.

Tunaheshimu Mamlaka kuliko siri za Mteja:Wakili Tigo
CAF yaichinja Biashara United Mara