Hatimaye Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limetegua kitendawili cha madai ya klabu ya Al Merrikh ya Sudan, ya kufanyiwa figisu walipokuwa nchini mwanzoni mwa mwezi huu, kwa ajili ya mchezo wa mzunguuko wanne wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi dhidi ya Simba SC.
Al Merrikh waliwasilisha malalamiko ‘CAF’ mnamo Machi 21 kulalamika figisu za kubambikiwa majibu ya vipimo vya virusi vya Corona kwa baadhi ya wachezaji wao, hali ambayo iliyowafanya kukosa mchezo dhidi ya Simba SC, uliomalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.
‘CAF’ wameijibu Al Merrekh kwa njia ya barua ambayo imeeleza kuwa, wanapaswa kuendelea na mipango yao kwa kuwa hakukuwa na hujuma zozote.
Barua hiyo imeeleza kuwa walipokea malalamiko hayo na utaratibu wa kupima Corona ulifuatwa na watu wa Simba SC hivyo kama hawajakubali kuhusu maamuzi hayo ni ruksa kwao kurejea tena ‘CAF’.
Simba SC wanaongoza kundi A ikiwa na alama 10 huku Al Merrikh wakburuza mkia wa kundi hilo kwa kumiliki alama moja baada ya kucheza michezo minne, imelazimisha sare mbele ya Simba Uwanja wa Al Hilal na imepoteza mbele ya AS Vita na Al Ahly ambazo zote zilifungwa na Simba SC.