Hatimaye Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limethibitisha kuwa Jumatano ya Desemba 21, itakua siku maalum ya kupanga Makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani humo.
‘CAF’ iliahirisha zoezi la upangaji Makundi ya Michuano hiyo ya ngazi ya vilabu Barani Afrika, lililokuwa limepangwa kufanyika Jumatano (Novemba 16) mjini Cairo Misri, bila kutoa sababu zozote.
Hata hivyo Shughuli zote za upangaji Makundi ya Michuano hiyo zimebaki nchini Misri mjini Cairo, ambako ndipo Makao Makuu ya Shirikisho hilo yalipo.
Vilabu 16 vilivyotinga hatua ya Makundi ya Michuano Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ni Al Ahly (Misri), Al Hilal (Sudan), Al Merrikh SC (Sudan), Atletico Petroleos (Angola), Coton Sport (Cameroon), CR Belouizdad (Algeria) na Esperance Tunis (Tunisia).
Nyingine ni Horoya (Guinea), JS Kabylie (Algeria), Mamelodi Sundowns (South Africa), Raja CA (Morocco), Simba SC (Tanzania), Vipers SC (Uganda), Wydad AC (Morocco), Zamalek (Misri) na AS Vita Club (RD Congo).
Vilabu 16 vilivyotinga hatua ya Makundi ya Michuano Kombe la Shirikisho Barani Afrika ni TP Mazembe (DRC), Pyramids (Misri), ASEC Mimosas (Ivory Coast), USM Alger (Algeria), Motema Pembe (DRC), Young Africans (Tanzania), AS FAR Rabat (Morocco) na US Monastir (Tunisia).
Nyingine Saint-Éloi Lupopo (DRC), Al Akhdar (Libya), Real Bamako (Mali), Rivers United (Nigeria), Diables Noirs (congo Brazzaville), Future (Misri), Marumo Gallants (Afrika Kusini) na ASKO Kara (Togo).