Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge imemhoji Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuhusu kauli yake ya “udhaifu wa Bunge.”
CAG amehojiwa mapema leo Januari 21, 2019 ambapo mara baada ya mahojiano hayo Mwenyekiti wa kamati hiyo, Emmanuel Mwakasaka amesema atawaeleza waandishi wa habari kilichojiri katika kikao hicho.
Prof. Assad ameitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa wakati akijibu swali la mwandishi wa televisheni ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda kuhusu kutoshughulikiwa ipasavyo kwa ripoti zake zinazoonyesha ufisadi.
“Kama tunatoa ripoti na kuna ubadhirifu na hatua hazichukuliwi huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa lisimamie na kuhakikisha kwamba pale kwenye matatizo hatua zinachukuliwa. Sasa sisi kazi yetu ni kutoa ripoti tu,” alisema CAG.
Aidha, katika mkutano wake na waandishi wa habari wiki iliyopita, Profesa Assad alionyesha kutaka busara zitawale suala hilo.
“Tunachoshauri sisi ni kwamba uungwana utawale katika mawasiliano yetu,” alisema Profesa Assad.
Alisema kauli yake haikulenga kulidhalilisha Bunge na kwamba neno udhaifu ni la kawaida hasa kwenye kada hiyo ya ukaguzi na amekuwa akilitumia hata katika ripoti zake.
Wakati hayo yakiendelea, Spika Ndugai alisitisha kufanya kazi na ofisi ya CAG na kuwatawanya wajumbe wa kamati mbili; ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuongeza nguvu kwenye kamati nyingine wakati huu ambao zitakuwa hazina majukumu.
PAC na LAAC zinazoongozwa na wenyeviti kutoka vyama vya upinzani, ndizo zimekuwa zikifanyia kazi ripoti za CAG na ratiba ya awali ya Bunge ilionyesha kamati hizo zingekuwa zikijadili ripoti ya sasa.
Prof. Assad aliteuliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, Desemba Mosi mwaka 2014 kuwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).