Picha: kutoka maktaba

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amekamilisha kazi ya kufanya uchunguzi wa fedha zilizochukuliwa Benki Kuu kati ya Januari – Machi, 2021 akieleza kuwa taratibu zilifuatwa.

Ripoti hiyo imetokana na maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Machi 28, 2021 alipokuwa akipokea Ripoti ya CAG ya Mwaka wa Fedha 2019/2020, Ikulu mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, CAG amemueleza Rais Samia kuwa utaratibu ulifuatwa katika kuchukua fedha hizo isipokuwa kulikuwa na mapungufu katika miamala iliyofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

“Mapungufu hayo ni pamoja na baadhi ya taasisi kama vile TANROADS na TPA kufanya malipo mara mbili kwa kazi moja au kuchelewa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya malipo ya kazi husika,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa mapungufu mengine ni kuchelewa kulipa wakandarasi, hatua ambayo imesababisha kuongezeka kwa riba kwenye malipo hayo na kuipa mzigo Serikali.

Mapungufu mengine kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni kutekeleza miradi ambayo haikuwa kwenye mpango, hivyo kufanya malipo nje ya Bajeti ya Serikali.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amepokea taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 2022. Majaribio ya Sensa hiyo yatafanyika Agosti mwaka huu.

Kutana na kijana aliyerudia darasa la kwanza kwa miaka 15, ana ndoto ya kuwa Rais
Ester Bulaya afunguka chama alichopo sasa, atoa ya moyoni kwa Rais Samia