Mshambuliaji wa pembeni wa Chelsea, Callum Hudson-Odoi amenusurika kwenda jela baada ya Polisi kumfutia shtaka la kubaka lililokuwa likimkabili.
Mwezi uliopita, Odoi mwenye umri wa miaka 20, alituhumiwa kumbaka mwanamke mmoja jijini London, tuhuma zilizopelekea ashikiliwe na Polisi na kisha baadae kuachiwa kwa dhamana, huku akiendelea kufanyiwa uchunguzi.
Hata hivyo, upelelezi uliofanywa na Polisi umebaini kuwa nyota huyo wa Chelsea hakufanya kosa hilo na sasa yuko huru.
“Mwanaume aliyeshikiliwa siku ya Jumapili, Mei 17, kufuatia tuhuma za kubaka, ameachiwa huru na hakuna hatua atakazochukuliwa,” ilisema taarifa hiyo ya Polisi.
Taarifa hizo zimeonekana kumpa furaha Odoi ambaye amesema kuwa kuanzia sasa atakuwa mfano bora kwa jamii.
“Napenda kuwashukuru wote walioonyesha kunisapoti katika nyakati ngumu.
Nimejifunza kwamba kuwa mwanasoka na kuchezea moja kati ya klabu bora duniani kunakuja na majukumu na kuanzia sasa na kuendelea, nitajitahidi kutumia nafasi yangu kama mchezaji wa Chelsea kuwa kioo kwa wengine,” alisema Odoi.
Msimu huu Odoi ameitumikia Chelsea katika michezo 27 ya mashindano mbalimbali, ambapo amefunga jumla ya mabao manne na kupiga pasi sita za mwisho.