Hasira za mkizi nusura zimpe hasara ya karne rapa wa kike Cardi B akijaribu kupambana na shabiki wa ‘hasimu’ wake Nicki Minaj aliyemtibua kwenye mitandao ya kijamii.
Rapa huyo wa kike mwenye umri wa miaka 25, mama wa mtoto Kulture, mtoto wa pekee aliyempata na mwanafamilia wa Migos, Offset hivi karibuni alisababisha Idara ya Huduma kwa Watoto kupigiwa simu ya dharura baada ya kutishia kumtupa mtoto wake chini ili azichape na shabiki wa Nicki Minaj.
Shabiki huyo wa Nicki Minaj aliandika kwenye Instagram akimchana Cardi B na dada yake Hennessy kuwa hata wafanye vipi hawataweza kufikia hatua aliyopo Nicki Minaj, akitumia maneno yenye ukakasi mzito.
Ingawa mkali huyo wa ‘Be Careful’ amekuwa akijiweka kando na kushambuliana na Nicki Minaj kwenye ngoma, aliamsha hasira na kumvaa shabiki huyo akimuelekeza sehemu aliyopo ili afike wazichape na kwamba atamtupa chini mtoto wake ili amfunze adabu shabiki huyo.
Cardi aliandika kwa hasira akieleza kuwa wakati huo yuko studio maeneo ya Atlanta akitumia maneno makali akimtaka shabiki huyo ajitokeze.
“F–k a @ I’m dropping my address is I’m in Atlanta in Mean studios wassup? PULL UP you claiming I’m p–y ? I;m giving you a LOCATiON any of ya in ATL? Cause im here and i drop my baby so i can fight RIGHT NOW !!!!” aliandika.
Hata hivyo, maneno hayo yanaonekana yametokana na hasira tu za muda za mwimbaji huyo kwani mapenzi ambayo amekuwa akiyaonesha kwa mtoto wake na kuyaweka wazi kwenye mitandao ya kijamii hayataruhusu kamwe kuiacha hata vumbi iguse unyayo wa mwanaye.
Nicki Minaj na Cardi B ambao wamekuwa wakitajwa kuwa mahasimu wakubwa, kwa nyakati tofauti wamekuwa wakieleza kuwa hawana ugomvi wowote na kwamba mashabiki ndio wanaochochea, wanaopika na kukoroga mambo yaonekane yalivyo.
Lakini mashabiki haohao, wiki hii wamekuwa wakishawishika kuwa Nicki Minaj amemtupia tena makombora Cardi B kwenye wimbo wake ‘Ganja Burns’ unaopatikana kwenye albam yake mpya ya ‘Queen’ iliyotoka Agosti 10. Nicki anasikika akiwashambulia wasanii wenzake wa kike akijigamba kumiliki taji la Umalkia wa muziki.