Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza vikao vyake leo kuyatathmini majina ya wagombea wa nafasi za ubunge kuelekea uchaguzi mkuu huku tarehe ya kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi hizo ikizidi kukaribia.
Katibu mkuu wa CCM, Bashiru Ally amesema wagombea wote wa ubunge na uwakilishi waliotia nia kwenye uchaguzi wa mwaka huu wanapaswa kusalia kwenye majimbo yao ya uchaguzi wakisubiri kufahamu hatma yao.
Chama hicho kinakuwa chama cha mwisho kuyatangaza majina ya wagombea wake wa nafasi zote za ubunge, uwakilishi na udiwani.
Chama hicho kinakabiliwa na mtihani wa kushughulikia vitendo vya rushwa zinazodaiwa kutawala wakati wa kura za maoni zilizofanyika kwa siku mbili katika wiki za hivi karibuni.
Wakati CCM ikiingia kwenye vikao vyake muhimu vya maamuzi kwa wagombea wa ubunge na uwakilishi vyama vingine vikuu vya upinzani Chadema na ACT Wazalendo vimevuka kipengele hicho na wagombea wake wameendelea kujitokeza wakichukua fomu.